Watoto wengi sana nchini Haiti wako katika hatari ya kifo huku magenge yakiimarisha nguvu zao na mzozo wa kibinadamu ukiwa mbaya zaidi, mkurugenzi wa shirika la Umoja wa mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) Catherine Russell alisema Jumanne.
Alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba “Ghasia na ukosefu wa usalama nchini Haiti vina athari kupita kiasi hatari ya ghasia zenyewe.”
Russell alisema zaidi ya watoto 125,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali, yote hayo “wakati vifaa vya kuokoa maisha viko tayari kutolewa ikiwa ghasia zitasitishwa na barabara na hospitali kufunguliwa.”
Kulingana na ripoti ya taasisi inayofuatilia usalama wa chakula Integrated Food Security Phase Classification initiative, takriban watu milioni 5 ambao ni nusu ya raia wa Haiti wamejikuta katika “viwango vya juu vya ukosefu mkali wa usalama wa chakula” tangu ghasia za magenge zilipoibuka.
Ukosefu wa usalama wa chakula na mzozo wa afya vinazidishwa na changamoto ya kuwafikia wale wanaohitaji msaada.