Njaa imeua watoto zaidi ya 400 nchini Sudan na kwamba huenda idadi hiyo ikawa kubwa zaidi, wakati huu mapigano yakiwa yameingia mwezi wa nne kati ya jeshi na wapiganaji wa RSF, imesema taarifa ya shirika la kimataifa, Save the Children.
Save the Children, limesema idadi hii inaweza ikawa zaidi kukiwemo makumi ya watoto waliokufa katika kituo cha serikali watoto yatima katika jiji kuu Khartoum.
Mkurugenzi wake nchini Sudan, Arif Noor, amesema hawakufikiria watashuhudia watoto wakifa kutokana na kile ambacho kingeepukika, wakati huu wakilazimika kufunga karibu vituo 57 vya lishe tangu vita kuanza.
Save the Children limesema watoto walioathirika zaidi ni walio chini ya miaka 5, wengi wakifariki kutokana na utapiamlo au magonjwa yanayohusiana nayo katika jimbo la kusini la White Nile.
Shirika hilo limeongeza kuwa zaidi ya watoto elfu 2 wamelazwa katika hospitali mbalimbali katika kipindi cha miezi minane wakiwa na utapiamlo mkali ambao ni aina mbaya zaidi ya utapiamlo.