Watoto zaidi ya 70 wamepoteza maisha kwa kipindi cha wiki tatu zilizopita nchini Sudan Kusini, kutokana na ugonjwa wa Surua.
Wizara ya afya inasema tangu kuanza kwa mwaka huu, ugonjwa huo umekuwa ukiripotiwa katika majimbo mbalimbali ya nchi hiyo, kama anavyoeleza Daktari Abdallah Faheem kutoka jimboni Jonglei.
‘‘Ugonjwa wa surua umezuka katika kaunti kadhaa na majimbo. Surua ilipozuka, magonjwa mengine kama kuharisha yanaweza kutokea. Motto anaweza kupata ugonjwa wa nimonia.
Surua inaambukizwa na kuenezwa haraka kutoka binadamu hadi binadamu mwingine.
Surua inasababishwa na virusi ambavyo vinaweza kubaki katika mazingara kwa masaa mawili hivi kwamba chembechembe za kuambukiza huenea na kuambukiza haraka.’’ alisema daktari Abdallah Faheem kutoka jimboni Jonglei.
Watalaam wa afya wanaonya kuwa iwapo watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, hawatopata lishe nzuri, itakayowasaidia kujikinga na ugonjwa huo, hali itaendelea kuwa mbaya.