Takriban watu tisa wameuawa na wengine zaidi ya 2,750, wakiwemo wanamgambo wa Hezbollah na matabibu, wamejeruhiwa wakati vifaa vyao vya kupeperusha ujumbe, Pager vilipolipuka kote Lebanon, vyombo vya habari na maafisa wa usalama wamesema.
Afisa wa Hezbollah, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba wanachama wa kundi hilo walijeruhiwa katika maeneo tofauti ya Lebanon na Syria wakati pager zao za mkononi zilipolipuka siku ya Jumanne.
Afisa huyo aliishutumu Israel kwa kulipua pager hizo, akiongeza kuwa huo ni “ukiukwaji mkubwa zaidi wa usalama” ambao kikundi hicho kilikumbana nacho katika takriban mwaka mmoja wa vita na Tel Aviv.
Wanamgambo wawili wa Hezbollah, akiwemo mtoto wa mwana wa mbunge wa Hezbollah, wameuawa na milipuko hiyo, vyanzo viwili vya usalama vililiambia shirika la habari la Reuters.
Kwa kuongezea, msichana mdogo pia aliuawa katika Wilaya ya Baalbek kaskazini mashariki mwa Lebanon, kulingana na vyombo vya habari vya Lebanon.
Ripoti hizo zinamtaja kama Fatima Jaafar Abdullah mwenye umri wa miaka 9, binti wa mwanachama wa Hezbollah.