Shirika rasmi la Habari la Sudan (SUNA) limeripoti kuwa watu 11 wamefariki dunia na wengine 60 kujeruhiwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha mafuriko katika mji wa Abu Hamad kaskazini mwa Sudan. Mvua hiyo imebomoa makumi ya nyumba huku timu za uokoaji zikiendelea kusaka watu waliotoweka na wengine walionasa chini ya vifusi.
Limeeleza kuwa kwa sasa haiwezekani kukadiria kikamilifu uharibifu uliosababishwa na mafuriko hayo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha ambazo zinazozuia mawasiliano kati ya maeneo ya Jimbo la Nile, lililoko umbali wa kilomita 400 kaskazini mwa mji mkuu, Khartoum.
Kwa upande wake, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limeripoti kwamba mvua kubwa na mafuriko ya Jumatatu na Jumanne ya jana, katika mji wa Abu Hamad ulioko karibu na Mto Nile, yamezilazimisha familia 86 kuhama makazi yao.
Taarifa ya IOM imesema kuwa nyumba 86 zimeharibiwa kabisa na nyingime 20 zimeathiriwa kwa kiasi na mafuriko hayo.
Mapema siku ya Jumatatu, Wizara ya Afya ya Sudan ilitangaza vifo vya watu 32 na kujeruhiwa wengine 107 kutokana na mvua kubwa iliyonyesha katika majimbo 7 ya nchi hiyo tangu mwezi wa Juni.
Maafa ya mafuriko mwaka huu yanaambatana na kuendelea kwa mateso yaliyosababishwa na vita kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) tangu katikati ya Aprili 2023, na kusababisha vifo vya takriban watu 15,000 na karibu milioni 10 kukimbia makazi, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa