Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, idadi ya vifo kutokana na mafuriko yanayoendelea nchini Somalia imeongezeka hadi 110, huku zaidi ya watu milioni moja wakikosa makazi.
Katika taarifa yake iliyotolewa jumapili, Ofisi hiyo pia imetoa tahadhari ya kutokea kwa magonjwa ya mlipuko kufuatia ripoti za kesi za watu wanaoshukiwa kuugua kipindupindu katika majimbo ya Hirshabelle na Galmudug.
OCHA imesema, boti 37 zimepelekwa kupeleka vifaa au kuwahamisha wale waliokwama na maji ya mafuriko.
Umoja wa Mataifa pia umeonya juu ya hatari kubwa ya kuenea kwa magonjwa kufuatia ripoti za kesi za watuhumiwa wa kipindupindu na kuhara kwa maji katika majimbo ya Hirshabelle na Galmudug.
Shirika hilo limeongeza kuwa ni asilimia 30 tu ya walioathirika ndio waliopokea msaada, lakini boti 37 zimepelekwa kupeleka vifaa au kuwahamisha wale waliokwama na maji ya mafuriko.
Katika wiki za hivi karibuni, Somalia na nchi jirani za Kenya na Ethiopia zimeshuhudia mvua kubwa zaidi katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili, na kusababisha vifo, kuhama makazi yao na uharibifu mkubwa.