Zaidi ya watu 110 waliuawa siku ya Alhamisi Oktoba 5, 2023 katika shambulio dhidi ya chuo cha kijeshi nchini Syria, wakati ambapo Uturuki ilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya Wakurdi ambayo yalisababisha vifo vya takriban watu 11.
Jeshi la Syria limehusisha shambulio hilo dhidi ya sherehe za kupandishwa vyeo kwa maafisa wa serikali huko Homs kwa”makundi ya kigaidi”.
Jeshi limeahidi “kujibu shambulizi hilo haraka iwezekanavyo”. Shambulio hilo lilitekelezwa “kwa kutumia ndege zisizo na rubani zilizojaa vilipuzi”, kulingana na jeshi.
Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 112, wakiwemo raia 21 na takriban 120 kujeruhiwa, kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Haki za Binadamu la Syrian Observatory for Human Rights (OSDH), shirika lenye makao yake nchini Uingereza lenye mtandao mkubwa kutoka vyanzo nchini Syria.
Waziri wa Afya wa Syria Hassan al-Ghobash alitangaza idadi “ya awali” ya watu 80 walioangamia katika shambulio hilo, “ikiwa ni pamoja na wanawake sita na watoto sita”, na karibu 240 kujeruhiwa.
Shambulio hilo halijadaiwa na kundi lolote. Makundi ya kijihadi yanayodhibiti sehemu ya ardhi ya Syria wakati mwingine hutumia ndege zisizo na rubani.