Takriban watu 12 wamepoteza maisha baada ya basi na lori kugongana uso kwa uso katika jimbo la kaskazini mwa Nigeria la Zamfara usiku wa kuamkia jana Alkhamisi.
Iro Danladi, Mkuu wa Kikosi cha Shirikisho cha Usalama Barabarani huko Zamfara ametoa taarifa hiyo leo mbele ya waandishi wa habari katika mji makao makuu ya jimbo la Zamfara yaani mji wa Gusau na kuongeza kwamba, watu wengine 13 wamepata majeraha ya viwango tofauti kwenye ajaili hiyo iliyotokea katika barabara ya Gusau-Funtua.
Danladi amewalaumu madereva kwa kuendesha magari kwa fujo na kwa kasi kubwa kupindukia na hivyo kusababisha magari hayo mawili makubwa yagongane uso kwa uso.
Amesema, majeruhi wote wa ajali hiyo ni abiria wa basi hilo ambalo lilikuwa limejaa kupita kiasi wakati wa tukio. Waliojeruhiwa wamepelekwa haraka katika hospitali ya eneo hilo kwa juhudi za samaria wema na maafisa wa usalama wa barabarani.
Ajali mbaya za barabarani huripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria, mara nyingi husababishwa na upakiaji kupita kiasi, hali mbaya ya barabarani, na kuendesha gari kwa uzembe.
Mwezi Januari mwaka huu, watu 15 waliteketea kwa moto baada ya basi moja kugongana na lori, kusini magharibi mwa Nigeria.