Watu kumi na watatu wanahofiwa kufa Maji Ziwa Victoria katika eneo la kijiji cha Mchigondo wilayani Bunda Mkoani Mara baada ya mitumbwi miwili kuzama ndani ya ziwa Victoria wakati watu hao wakitoka kanisani.
Habari kutoka Mkoani Mara zinasema katika tukio hilo Mwili wa mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa mwaka mmoja umeopolewa kutoka ziwani huku wengine kumi na wanne wameokolewa katika ajali hiyo iliyohusisha mitumbwi miwili.
Mkuu wa wilaya ya Bunda, Dk.Vicent Naano amethibitisha tukio hilo la kuzama mitumbwi lililotokea jioni wakati watu hao walipokuwa wakitoka kusali katika kijiji cha Ichigondo wilayani humo.
Kulingana na Mkuu huyo wa wailaya ya Bunda Kijiji cha Igundu kuna Ras ambapo baadhi ya watu hutumia usafiri wa mitumbwi kwenda au kutoka kanisa la KTMK na kufafanua kuwa katika tukio hilo mtumbwi mmoja ulipigwa na dhoruba na kuanza kuzama ndipo mtumbwi wa pili ulikwenda pale kuwaokoa nao ukapigwa na dhoruba na yote miwili ikazama.
Aidha katika ajali hiyo watu 14 wameokolewa na wengine kumi na watatu wanaendelea kutafutwa huku kukiwa na hofu wamekufa maji.