Mazishi ya Mwanamfalme na mume wa Malkia wa Elizabeth II, Prince Philip yanafanyika leo huku watu 30 tu ndio wameorodheshwa kushiriki kwenye shughuli hiyo. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Buckingham, ibada ya mazishi itaanza saa 11 jioni huku watoto wanne wa Mwanamfalme huyo watalisindikiza jeneza la baba yao katika shughuli hiyo.
Watoto hao ni Charles, Andrew, Edward, Anne na wajukuu wake, Prince William na Harry watakuwa wakitembea pembezoni mwa magari maalumu yatakayokuwa na mwili huo. Ibada ya mazishi itafanyika Kanisa la Mtakatifu George katika kasri ya Windsor.
Idadi ya watu walioalikwa kushiriki mazishi hayo ni 30, wakiwamo ndugu watatu wa Philip kutoka Ujerumani. Wageni wote watavalia barakoa na hawatakaribiana kama inavyoelekezwa katika mwongozo wa kudhibiti virusi vya corona. Malkia Elizabeth atakaa hema la peke yake.
Msiba huo ndio umewakutanisha tena ndugu wawili, Prince William na Harry ambaye alijiondoa katika hadhi ya kifalme na sasa ameweka makazi yake Marekani.