Shambulizi la Israel kwenye jengo la mji wa Gaza limeua watu 76 wa familia moja, msemaji wa Idara ya Ulinzi ya Raia wa Gaza amesema.
Mlipuko wa siku ya Ijumaa unaaminika kuwa miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya vita hadi sasa, kulingana na Mahmoud Bassal.
Alisema wakuu wa kaya 16 kutoka familia ya al Mughrabi waliuawa, pamoja na wanawake na watoto.
Miongoni mwao alikuwa Issam al Mughrabi, mfanyakazi wa muda mrefu wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, mke wake, na watoto wao watano.
Katika taarifa kutoka kwa shirika hilo, walithibitisha kuwa mzee huyo mwenye umri wa miaka 56 alikufa pamoja na mkewe Lamya’a, 53, na watoto Mohammad, 32, Saud, 30, Lama, 27, Luai, 23, na Obaideh, 13.
“Kwa karibu miaka 30, Issam amefanya kazi na UNDP kupitia Mpango wetu wa Msaada kwa Watu wa Palestina. Atakumbukwa kama mwanachama mpendwa wa timu ya PAPP,” ilisema.
“Kupoteza kwa Issam na familia yake kumetuathiri sana sisi sote. Umoja wa Mataifa na raia huko Gaza sio walengwa.”
Zaidi ya watu 20,000 huko Gaza sasa wanaripotiwa kufariki tangu tarehe 7 Oktoba. Takriban watu 1,200 wamekufa nchini Israel.