Serikali ya Burundi imesema takriban watu tisa wakiwemo wanawake sita na mwanajeshi mmoja, wameuawa katika kijiji cha Buringa karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) .
Msemaji wa serikali ya Burundi Bw. Jerome Niyonzima amesema waasi wa kundi la RED-Tabara walifanya shambulizi hilo ambalo pia lilijeruhi watu watano. Waasi hao pia walilenga ofisi ya chama tawala cha CNDD-FDD katika eneo hilo.
Kundi la RED-Tabara limedai kuhusika na shambulio hilo likisema lililenga vituo viwili vya kijeshi huko Buringa, na kusababisha vifo vya wanajeshi sita, kuharibu ofisi ya chama cha CNDD-FDD, pamoja na kukamata silaha na risasi.
RED-Tabara ni kundi la waasi lililoko mashariki mwa DRC na limekuwa likipambana na serikali ya Burundi tangu 2015.