Watu watano wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika shambulizi linaloshukiwa kufanywa na waasi wa kundi linalojiita Allied Democratic Forces (ADF) magharibi mwa Uganda.
Shirika la habari la Reuters lilitangaza habari hiyo jana Jumanne na kueleza kuwa, waasi wa ADF walifanya mauaji hayo baada ya kushambulia kijiji cha Kyabandara ambacho aghalabu ya wakazi wake ni Wakristo katika Wilaya ya Kamwenge, magharibi mwa Uganda.
Mbunge katika eneo hilo, Cuthbert Abigaba, amenukuliwa na Reuters akisema kuwa, miongoni mwa watu waliouawa katika shambulio hilo la wanamgambo wa ADF ni diwani wa eneo hilo.
Msemaji wa Jeshi la Uganda, Deo Akiiki amethibitisha habari za kutokea shambulio hilo. Habari zaidi zinasema kuwa, wapiganaji wa ADF mbali na kufanya mauaji katika eneo hilo, lakini pia walichoma moto mgahawa na kuiba kwenye maduka kadhaa.
Waasi wa ADF wamekuwa wakiendesha harakati zao kwenye misitu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrsia ya Kongo kwa zaidi ya miongo miwili sasa, na wamekuwa wakifanya mashambulizi ndani ya nchi hiyo na wakati mwingine ndani ya ardhi ya Uganda. Wapiganaji wa ADF
Mwezi uliopita, Jeshi la Uganda lilitangaza kuwa limeua waasi sita wa ADF na kumkamata kamanda anayeaminika kuhusika na mauaji ya watalii wawili wa kigeni na mwongozaji wao raia wa Uganda katika mbuga ya wanyama ya magharibi mwa nchi hiyo iliyoko karibu na mpaka wa DRC.
Kabla ya hapo, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda alitangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limeua kwa akali wapiganaji 560 wa kundi la kigaidi la ADF.
Jeshi la Uganda UPDF kwa kushirikiana na jeshi la Kongo DR limekuwa likipambana na makundi ya wabeba silaha kwa karibu miaka miwili sasa.