Watu Sita wanashikiliwa na Polisi wakituhumiwa kuficha Kwa kuwahifadhi wahalifu walioingia kinyemela na kujihusisha na uchimbaji wa madini eneo ambalo ni chanzo tegemeo cha Maji kwa wakazi zaidi ya 22,000 wa kata nne za Vudee,Mwembe,Mhezi na Mbangalala Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao Sita ni matokeo ya Oparesheni ya kamati ya Usalama Wilaya ya Same iliyo ongozwa na mwenyekiti wake ambae ni mkuu wa Wilaya Kasilda Mgeni, waliolazimika kufanya msako kwa kushtukiza baada ya kupata taarifa za kuwepo watu zaidi ya 70 wanaoendesha shughuli za uchimbaji madini Aina ya Dhahabu bila vibali.
Kwa mujibu wa mkuu wa Wilaya ya Same taarifa zilizo mfikia ni kwamba mbali na wachimbaji hao kufanya shughuli zao kinyemela, pia wameharibu miundombinu ya Maji na kuhatarisha Usalama wa watumiaji kwakua wanasafisha madini moja Kwa moja kwenye Bwawa wakitumia Mercury ambayo ni hatari kwa binadamu.
“Kuingia huku kinyemela na kuharibu miundombinu ya Maji NI hujuma, hatutavumilia vitendo kama hivi, niwatake Jeshi la Polisi kuweka kambi kwenye eneo hili kuimarisha ulinzi kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinakoma na waliohusika kuihujumu Serikali lazima watafute popote na wachukuliwe hatua”.Alisema Kasilda Mgeni mkuu wa wilaya ya Same.
Awali kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mteke Felix Ngeti amesema kwa sasa asilimia kubwa ya watu wamelazimika kuacha kutumia Maji hayo kwakua Uharibifu ni mkubwa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi kulazimika kutafuta huduma ya majinsafi maeneo ya mbali.
“Hapa mnapoona kuna wachimbaji zaidi ya sabini na viongozi wa kijiji walikuja baada ya kupata malalamiko kwa wananchi juu ya uchaguzi unaofanyika lakini wachimbaji hao kwakua waliokua wengi waliwafukuza viongozi”.Alisema Ngeti.
Baadhi yao wakazi wanaoishi jirani na eneo hilo kulikofanyika Uharibifu wamepongeza hatua za haraka zilizochukuliwa na kamati ya Usalama, wakisema Hali ilizidi kuwa mbaya kwakua kumekua na ongezeko la idadi ya watu wanaotoka maeneo mbalimbali na kuingia kinyemela katika eneo hilo la chanzo cha Maji na kuanza uchimbaji wa madini.