Takriban watu 20 wamekufa maji baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama kwenye Mto Benue wa katikati mwa Nigeria.
Serikali ya eneo hilo imethibitisha habari hiyo na kusema kwamba, ajali hiyo ilitokea katika jimbo la Benue wakati wafanyabiashara walipokuwa wanarejea kutoka kwenye gulio la kila wiki.
Melvin James mmoja wa maafisa wa serikali ya eneo hilo amesema: “Baadhi ya watu hawajulikani walipo hadi hivi sasa.”
Ameongeza kuwa, hadi wakati anatangaza habari hiyo, wapiga mbizi wa eneo hilo walikuwa wanaendelea na juhudi za kuwatafuta na kuwaokoa watu waliopotea.
Mmoja wa watu walioshuhudia ajali hiyo amesema kuwa, wahanga wengi walikuwa ni wanawake na watoto wadogo.
Ajali za boti hutokea mara kwa mara nchini Nigeria, mara nyingi husababishwa na upakiaji wa abiria na mizigo kupita kiasi, hali mbaya ya hewa, na hitilafu za ufundi kutokana na uchakavu wa vyombo vya kusafiria.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Novemba, karibu watu 27 walipoteza maisha baada ya boti kuzama katika Mto Niger ulioko katikati mwa Nigeria.