Watu wasiopungua 29 wamefariki na wengine zaidi ya laki 8.5 wamekimbia makazi yao kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini Somalia.
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetahadharisha kuwa maafa ya mafuriko yanaweza kutokea katika sehemu zote za Somalia kutokana na mvua kubwa inayoendelea, na kuwaathiri watu milioni 1.2 wanaoishi kando ya mito.
Mvua kubwa imekuja baada ya Somalia kukumbwa na ukame mkali ambao haukuwahi kushuhudiwa katika miongo minne iliyopita. Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa hivi sasa zaidi ya watu milioni 3.7 wanakabiliwa na njaa kali nchini humo, na huenda idadi hiyo ikaongezeka hadi milioni 4.3 ifikapo mwezi Disemba kutokana na mafuriko.