Zaidi ya maafisa wa polisi 15 na raia kadhaa, akiwemo kasisi wa Kanisa la Orthodox, waliuawa na wanamgambo wenye silaha katika jamhuri ya kusini ya Urusi ya Dagestan siku ya Jumapili, gavana wake Sergei Melikov alisema katika taarifa ya video mapema Jumatatu.
Watu hao wenye silaha walifyatua risasi makanisa mawili ya Orthodox, sinagogi na kituo cha polisi katika miji miwili, kulingana na mamlaka.
Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi ya Russia imeyataja mashambulio hayo katika eneo hilo lenye Waislamu wengi wenye historia ya uasi wa kutumia silaha kuwa ni vitendo vya kigaidi.
Jumatatu, Jumanne na Jumatano zilitangazwa kuwa siku za maombolezo katika eneo hilo.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Dagestan ilisema kundi la watu wenye silaha walipiga risasi kwenye sinagogi na kanisa katika jiji la Derbent, lililoko kwenye Bahari ya Caspian. Kanisa na sinagogi zilishika moto, kulingana na vyombo vya habari vya serikali. Karibu wakati huo huo, ripoti zilionekana kuhusu shambulio la kanisa na kituo cha polisi wa trafiki katika mji mkuu wa Dagestan, Makhachkala.
Mamlaka ilitangaza operesheni ya kukabiliana na ugaidi katika eneo hilo. Kamati ya Kupambana na Ugaidi ilisema watu watano wenye silaha “waliondolewa.” Gavana alisema “majambazi” sita “wamefutwa.” Idadi hizo zinazokinzana hazikuweza kusuluhishwa mara moja na haikubainika ni wanamgambo wangapi walihusika katika mashambulizi hayo.