Idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa kusini mashariki mwa Morocco imeongezeka na kufikia watu 18.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco imebainisha kuwa, watu kumi wamepoteza maisha katika jimbo la Tata, na wawili huko Tiznit na watatu katika eneo la Errachidia.
Raia watatu wa kigeni ni miongoni mwa wahanga wa mafuriko ya Morocco.
Watu wanne hawajulikani walipo katika jimbo la Tata huku nyumba na barabara zikibomolewa kwa mafuriko.
Rachid al Khalifi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco jana alieleza kuwa kiasi cha mvua kilichorekodiwa siku mbili zilizopita ni sawa na karibu nusu ya mvua zinazonyesha kila mwaka huko Morocco.
Nyumba 24 zimekobolewa, 16 zimeharibika kwa upande mmoja na barabara 93 zimepata hasara kubwa na hivyo kusababisha tatizo la usafiri.
Wakati huo huo umeme, huduma ya maji ya kunywa na mitandao ya simu pia imeathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha Morocco tangu juzi Jumapili.