JUHUDI za serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia zimezidi kuungwa mkono baada ya Kampuni ya Gesi ya Oryx Tanzania kuingia mkataba na Taasisi ya Doris Mollel, kuwapatia mitungi na majiko ya gesi wauguzi kutoka mikoa 10 nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutia saini makubaliano hayo leo Aprili 19, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Kinondoni Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Oryx, Benoite Araman amesema lengo la hatua hiyo ni kutanua matumizi ya nishati ya kupikia katika jamii.
Araman amesema matarajio ya Kampuni hiyo ni kuhakikisha kila Mtanzania anatumia nishati safi ya kupikia.
“Kunahitajika elimu ya kuhakikisha watu wanaokolewa dhidi ya matumizi ya nishati isiyofaa, tunatarajia kutoa majiko mengi zaidi na hadi sasa tumeshatoa majiko 32,000,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation, Doris Mollel amesema lengo la kulifikia kundi la wauguzi anya ni kuhakikisha wanawaepusha na athari za matumizi ya nishati chafu ambayo ina madhara kwa jamii.
Doris, ameeleza ugawaji wa majiko hayo utawagusa wauguzi katika mikoa
“Tunatambua nafasi ya wauguzi wa afya, wamekuwa na mchango mkubwa kwenye jamii, tunaona makundi mengine yakipewa majiko sisi tunaona ni muhimu tuwape wauguzi,” ameeleza.
Amebainisha kuwa, majiko hayo yatakabidhiwa kwa wauguzi walio katika mazingira magumu kuwaepusha na matumizi ya nishati yenye madhara
Mganga Mfawidhi wa Hospitali yaMwananyamala, Zavery Benela amesema matumizi ya nishati chafu ni moja ya sababu ya magonjwa mengi ya mfumo wa hewa kwa binadamu.
Ameeleza kati ya wagonjwa 500 wa nje wanaopokelewa katika hospitali hiyo, zaidi ya nusu wanasumbuliwa na magonjwa ya mfumo wa hewa.
“Haya ndiyo magonjwa namba moja kwa wagonjwa wengi kwenye hospitali yetu, tumekuwa tukiwapokea na ukiuliza namna anavyoishi utakuta anatumia nishati isiyofaa kupikia,” ameeleza.