Wawekezaji wa sekta ya viwanda wametakiwa kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali ya kazi nchini ikiwemo kuboresha mifumo ya usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi ili kuwalinda wafanyakazi dhidi ya athari wanazoweza kuzipata wakiwa kazini.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maenedeleo ya Jamii ya kutembelea viwanda Mkoani Arusha akiambatana na kamati hiyo ili kujionea utekelezaji wa sheria na miongozi mbalimbali ya kazi ikiwemo Sheria Na.5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2003.
“Kwanza kabisa tunapenda wawekezaji waje nchini kwa wingi na wanapowekeza basi waendeshe shughuli zao zote kwa kuzingatia sheria mbalimbali za nchi ikiwemo sheria na miongozo mbalimbali ya kazi, huwa tunafurahi sana tunapoona wawekezaji wanatengeneza ajira kwa vijana wetu lakini pia wakiendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria za nchi “ alisema Prof. Joyce Ndalichako.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ustawi na Manendeleo ya Jamii, Mhe. Riziki Saidi Lulida amewataka wawekezaji hao kuhakikisha wanaweka miundo mbinu rafiki katika maeneo mbalimbali ya viwanda vyao kwa watu wenye ulemavu.
“Tunazo sheria za nchi zinazoelekeza viwanda kujenga miundo mbinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, kwa mfano mimi leo nimeshindwa kuingia ndani katika baadhi ya viwanda tulivyotembelea kutokataka na ulemavu wangu wa miguu kwasababu maeneo mengi yana ngazi, naamini kuna wafanyabishara wengi wenye ulemavu ambao pengine wanatamani kuingia katika maeneo ya viwanda na wakashindwa kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki kwao hivyo wito wangu kwa wawekezaji wote nchini katika sekta hii ya viwanda waboreshe miundommbinu ili kuwapa fursa wenye ulemavu” alisema Makamu Mwenyekiti, Bi. Riziki Saidi.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo na Mbunge wa Jimbo la Jang’ombe, Mhe. Ali Hassan King ameishauri taasisi ya OSHA kuendelea kuimairisha mifumo ya usimamizi wa usalama na afya katika ameneo ya kazi nchini huku akiahidi kuwa wataendelea kuishauri serikali juu ya uimarishaji wa mifumo ya usalama na afya katika viwanda.
“Kupitia ziara hii tumepata mengi ya kujifunza na kuishauri serikali na katika maeneo yote tuliyotembelea kwa kiasi kikubwa tumeridhishwa na hali ya utekelezaji wa sheria na miongozo ya usalama na afya na kuna mambo mbalimbali tumehoji katika viwanda hivi na tumewaelekeza kutoa majibu kwa kuandikia taarifa nasisi tutaiandikia ripoti ili kuiwasilisha bungeni kwa lengo la kuishauri serikali” alisema Mhe. Ally Hassan
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi wa OSHA, Dkt. Jerome Materu amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa sana kwa wawekezaji wote kuzingatia taratibu na miongozo yote ya usalama na afya kwasababu huongeza tija na kupunguza gharama za uendeshaji wa maeneo yao ya kazi.
“Unapowekeza katika masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kuna mahusiano makubwa kati ya upunguzaji wa gharama na uendeshaji wa eneo la kazi hivyo tunaishukuru sana Kamati hii ya Bunge kwasababu na wao wamekuwa ni jicho la tatu katika kuangalia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi na wametupatia ushauri ambao tutautumia katika kuboresha usimamizi wa mifumo ya usalama na afya katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini “ alisema Dkt. Jerome Materu
Aidha wawakilishi wa viwanda vilivyotembelewa wameishukuru kamati hiyo kubainisha kuwa ziara hiyo imewapa funzo kubwa huku wakiahidi kuendelea kuboresha zaidi mifumo ya usimamizi ya usalama na afya mahali pa kazi.
Katika Ziara hiyo Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendelea ya Jamii imetembelea viwanda vitatu Mkoani Arusha ambavyo ni: Kiwanda cha kuzalisha Transifoma cha TANELEC Limited, Kiwanda cha kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo nguo cha A to Z Textiles Mills Ltd pamoja na kiwanda cha maua cha Fides Tanzania.