Naibu katibu mkuu Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia DK Franklin Rwezimula amewataka wawezeshaji kitaifa wa mtaala wa elimu ya awali nchini kuzingatia mafunzo kwa umakini kwani mtaala unatarajiwa kuanza mwaka 2024 kwa ngazi ya elimu ya awali na msingi ili kuwawezesha walimu kutekeleza mtaala kwa weledi.
Akifungua mafunzo hayo leo katika chuo cha Kleruu kilichopo mkoani Iringa Dk Rwezimula amesema ili mitaala itekelezwe kwa ufanisi ni lazima kuwe na walimu wenye weledi katika ufundishaji na amewataka wawezeshaji hao wazingatie mafunzo wanayopatiwa ili waweze kufanya kazi ya uwezeshaji vyema
Ameendelea kusema kuwa wizara inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuboresha mafunzo endelevu kazini ili kuhakikisha walimu wanakuwa bora katika maeneo ya kazi ikiwemo uboreshwaji wa mazingira ya kazi , kwa kuboresha miundombinu na vifaa vya kujifunzia na kufundisha ikiwemo vifaa vya Tehama .
Mkurugenzi wa TET Dkt . Aneth Komba amesema kuwa mitaala imefanyiwa maboresho makubwa ikiwemo muundo wa elimu , matumizi ya Tehama kuanzia ngazi ya awali kwa namna ya utumiaji na ufundishaji na elimu ya ya awali itatanguliwa na elimu ya malezi na makuzi itakayotolewa kwa watoto
Mafunzo haya yatafanyika katika maeneo mbalimbali ambapo mafunzo haya awamu ya kwanza yameanza kufanyika mkoani Iringa na baadae itaendelea mikoa mingine.