Polisi Mkoa wa Njombe imethibitisha kifo cha Golden Doglas Luoga (34) aliyekuwa Mfanyabiashara wa miamala ya fedha katika Halmashauri ya Mji wa Njombe kilichotokea wakati akiendelea kupata matibabu baada ya kupigwa risasi na Watu wawili wanaodaiwa kuwa ni Majambazi waliomvamia nyumbani kwake katika eneo la Galuhenga lililopo Mtaa wa Kambarage.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe John Makuri Imori amesema wamepata taarifa za kifo cha Golden Luoga wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya alikohamishiwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
“August 29 mwaka huu usiku kule katika Mtaa wa Kambarage, Majambazi wawili waliokuwa na silaha za moto walimvamia Golden Luoga sasa pale kwake alikuwa pia na Ndugu yake anaitwa Faraja Luoga yeye ana miaka arobaini”
“Wote walijeruhiwa kwa risasi na wakati wanakimbizwa Hospitali Faraja alifariki lakini Golden yeye akawa anaendelea vizuri na alihamishwa kutoka kwenye Hospitali yetu hapa na kupelekwa kwenye Hospitali ya Rufaaa Mbeya lakini akafariki alfajiri jana”