Watu wawili wamefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa wakiitumia kugonga lori kwa nyuma lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara kutokana na tairi kupata pancha.
Tukio hilo limetokea barabara kuu ya Arusha-Babati ambapo pikipiki yenye namba za usajili MC 509 BDK iligongha gari hiyo yenye namba za Usajili T.336 AFE ambayo ni mali ya Siara Laizer.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Banjamin Kuzaga amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Dereva wa pikipiki hiyo Daudi Jumanne (25) mkazi wa kijiji cha Magugu na Hussein Mustapha (21) mkazi wa kijiji cha Kiongozi tukio lililotokea Januari 2,2022 katika kijiji na kata ya Magugu wilayani Babati mkoani Manyara.
Katika tukio lingine jeshi la Polisi mkoani Manyara limeeleza kuwa mnamo Januari 1,2022 katika Kitongoji cha Ngage Jangwani Wilayani Simanjiro mtu mmoja aliefahamika kwa jina la Riziki Enock (34) alijeruhiwa kwa kuchomwa na kisu kifuani na mke wake aitwaye Mwanaisha Selemani (26), majeruhi amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi kwa matibabu zaidi huku mtuhumiwa akishikiliwa na Polisi.