Wazazi wameshauriwa kutowalea watoto wao kwa kuiga tamaduni za kimangharibi zinazopelekea mmomonyoko wa maadili yakiwemo mapenzi ya jinsia moja na badala yake wawalee kwenye misingi ya tamaduni za kitanzania zitakazowajengea watoto uwezo wa kufanya kazi,kujitambua na kuwa na hofu ya Mungu.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la kutetea haki za watoto na kupinga ukatili wa kijinsia la Nelico wakati wa mahafali ya 11 ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Geita Adventist iliyopo mjini Geita.
Amesema mmomonyoko wa maadili uliopo sasa umechangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wazazi au walezi wanaoishi maisha ya ‘usasa’kwa kuiga tamaduni za kimangharibi zinazofanya watoto wakue wakiamini ndio malezi sahihi hivyo kusahau mila na tamaduni za kitanzania zinazomjenga mtoto kuwa na hofu ya Mungu,kufanya kazi na kuwa na heshima kwa jamii nzima.
“Zamani mtoto wa mwenzako alikua wako na wajamii nzima lakini sasa imebadilika kila mtu anaangalia wa kwake tumesahahu malezi,maadili yameporomoka na ndio maana sasa tunapambana na mapenzi ya jinsia moja hii imetokana na sisi wazazi kushindwa kuwaonya watoto wetu”amesema Paulina.
Amesema watoto wanapitia changamoto mbalimbali za ukatili wa kingono,kijinsia na kisaikolojia na kwamba bila kuwa na malezi sahihi yenye hofu ya Mungu sio rahisi kushinda changamoto zilizopo kwa sasa.
Mkurugenzi wa Shule za Geita Adventist George Hezron akizungumza kwenye mahafali hayo yaliyohusisha wahitimu 234 wa kidato cha nne, amesema shule hiyo inawalea watoto kwenye maadili ya kiroho yanayowapa uwezo wa kukabiliana na changamoto ya utandawazi kwenye jamii na hata kama wataenda nyumbani pia itasaidia maan walishapata elimu.
“Kwa sasa changamoto kubwa ni utandawazi na mitandao ya kijamii imekuwa ngumu kwa watoto kuchagua kipi bora kwa maisha yao ya kesho.Sisi tunajitahidi kuwafundisha kujitambua,kujua haki zao tunatoa malezi ya kiroho na kuwafanya wajue Imani ya dini ambayo itawasaidia kujua dhambi ni mbaya”amesema Hezron
Akizungumzia maandalizi ya mtihani wa kitaifa Mkurugenzi huyo amewataka wanafunzi wawe waadilifu,waepuke udanganyifu kwenye chumba cha mitihani kwakua mdhara yake ni makubwa kwa mwanafunzi mwenyewe,shule na hata jamii nzima.
Akizungumza kwa niaba ya wazazi ambao watoto wao wamehitimu shuleni hapo,Juma Jumanne amesema ulegevu wa wazazi kutozingatia malezi waliyopewa na wazazi wao zamani ndiko kunakopelekea mmomonyoko wa maadili ulioko kwenye jamii kwa sasa.