Waziri wa Polisi nchini Madagascar Serge Gelle (57) amenusurika kifo baada ya helikopta aliyokuwemo kupata ajali baharini Jumatatu.
Gelle ambaye alikuwa polisi kwa miaka 30 kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri hivi karibuni, aliogelea kwa masaa kumi na mawili kabla ya kufika nchi kavu katika mji wa Mahambo siku ya Jumanne.
Waziri huyo alitumia kiti kimoja cha helikopta kama kifaa cha kumsaidia kuelea.
Gelle na wafanyakazi wenzake wawili walikuwa wakikagua eneo lililoko Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo ambako kulitokea ajali ya boti ya abiria iliyoua watu wapatao 39 na wengine wengi kupotea.
Zoezi la uokoaji wa ajali hiyo ya boti bado linaendelea.