Mkutano huo umefanyika tarehe 16 Aprili 2024 jijini Dodoma na kuwakutanisha Wakulima, Wazalishaji, Viongozi wa Vyama vya Ushirika, Wamiliki wa Viwanda vya Uchakataji, Wafanyabiashara, Waheshimiwa Wabunge kutoka Mikoa inayozalisha zao la Kahawa; Mhe. Ng’wasi Kamani (Mb), Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, na Mhe. Mariam Ditopile Mzuzuri (Mb), Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo.
Waziri Bashe amesema kuwa kwa sasa uzalishaji wa zao la Kahawa umefikia tani 80,000. “Lengo letu ni kuzalisha tani 300,000 za kahawa hadi ifikapo mwaka 2030. ‘We must justify our failures.’ Hatuna sababu ya kutokuwa na maamuzi na kutekeleza. Kheri kujaribu kwa nia njema kuliko kutokujaribu.”
Mhe. Bashe amesema kumekuwa na makelele kwa Wakulima kuhusu Ushirika kwa kubambikiwa riba za mikopo ya pembejeo za kilimo hivyo amevitaka Vyama vya Ushirika kukusanya mahitaji ya wanachama wao, ili Serikali kupitia Bodi ya Kahawa iwapatie mahitaji yao.
“Kuna matatizo mengi sana kwenye Kahawa na yote yanatokana na ulimbikizaji wa tozo zisizo na msingi wowote na kuleta ukandamizaji kwa Wakulima. Lazima tubadilishe mfumo,” amesema Waziri Bashe. Serikali inapitia upya mnada wa Kahawa kuanzia shambani kwa Mkulima mpaka kufika sokoni ili kumuwezesha mkulima kunufaika na zao la Kahawa.
Aidha, Waziri Bashe amemuagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa kuhakikisha zoezi la kuwachimbia visima wakulima linafanyika haraka ili kuwahakikishia kilimo cha uhakika na kuzalisha kwa tija.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Mariam Ditopile (Mb) amesema Kamati inaungana na Wizara ya Kilimo katika mpango wa kuongeza bajeti ya Wizara hiyo na kuhakikisha kuwa fedha zinafika kwa wakati ili kutekeleza mipango ya kuboresha kilimo nchini kwa manufaa mapana ya Wakulima.