Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amezindua Ofisi za Benki ya Meandeleo ya Kilimo(TADB) Kanda ya Magharibi huku akitumia nafasi hiyo kueleza umefika wakati wa kuwa na sera ya fedha katika kilimo lengo likiwa kuwawezesha wakulima kupata mikopo yenye riba nafuu tofauti na ilivyosasa ambapo wanakopa katika benki zenye mlengo wa kibiashara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi za Benki ya TADB Kanda ya Magharibi Mjini Tabora , Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kanda hiyo inajumuisha Mkoa wa Tabora, Kigoma na Katavi na uwepo wa ofisi za benki hiyo katika kanda hiyo inakwenda kusogeza huduma karibu na wakulima.
Akielezea zaidi kuhusu mikakati ya Serikali katika kilimo amesema pamoja na mambo mengine iko haja ya kuwa na sera ya fedha itakayohusu sekta ya kilimo ambayo itatoa fursa ya wakulima kuwa na uwezo wa kukopesheka kwa urahisi na bila ya kuwepo kwa vikwazo ambavyo vinasababishwa na kutokuwepo kwa sera ya fedha katika kilimo.
“Jambo la pili ambalo nataka niseme na kwa kuwa mwakilishi wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT) yuko hapa , mikopo katika sekta ya uchumi wa nchi yetu uchumi wote mikopo inayoingia ni zaidi ya Sh.trilioni 20 na inayokwenda sekta ya kilimo ni asilimia chini ya 10…
“Na bado ukienda kwenye uzalishaji katika kilimo fedha inayotolewa kama mkopo ni ndogo sana.Sasa hoja yangu na nimeshaongea na Waziri wa Fedha , Gavana wa Benki Kuu , Waziri wa Mipango na ninawaandikia barua.
“Tunahitaji sera ya fedha ya kilimo kwani haiwezekani kilimo kikopeshwe kwa kutumia sera za benki za biashara.Kutumia sera hiyo bado hatutoweza kutoa watu kwenye umasikini,” amesema Waziri Bashe.
Ameongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada kubwa katika kuinua sekta ya kilimo na kuboresha maisha ya wakulima akitolea mfano ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya kilimo cha umwagiliaji unaofanywa na Serikali.
“Serikali ikashamaliza kuboresha miundombinu mkulima anahitaji fedha ya kununua mbolea , pembejeo na mambo mengine yanayohusu kilimo.Kwa hiyo ni muhimu tukawa na sera ya kupata mitaji kwenye sekta za uzalishaji kilimo, mifugo na uvuvi.”