Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeshiriki kikamilifu kwenye kilele cha Maadhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi iliyopo mkoani Morogoro huku ikiahidi kuendelea kubuni huduma mbalimbali za kifedha mahususi kwa wadau sekta ya utalii nchini.
Hatua inalenga kuunga mkono jitihada za serikali katika kuvutia idadi kubwa ya watalii wanaokuja nchini kupitia uwepo wa huduma bora kifedha kwa wadau wa sekta hiyo wakiwemo watalii.
Dhamira ya benki hiyo iliwekwa wazi na Meneja Maendeleo ya Biashara tawi la Morogoro, Joseph Boaz mbele Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) wakati waziri huyo alipotembelea banda la maonesho ya benki hiyo lililokuwepo kwenye viunga vya maadhimisho hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye uwanja wa mpira wa Kikoboga uliopo kwenye hifadhi hiyo. Benki ya NBC ilikuwa ni moja ya wadhamini muhimu wa maadhimisho hayo.
Kwa mujibu wa Boaz, ushiriki wa benki hiyo kwenye maadhimisho hayo kwa kiasi kikubwa unachagizwa na ushirikiano mkubwa uliopo baina yake na wadau mbalimbali wa utalii nchini likiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), wafanyakazi wa shirika hilo, wadau wa utoaji huduma za utalii pamoja na watalii wanaotembelea hifadhi mbalimbali nchini ikiwemo ya Mikumi.
“Ni kutokana na ushirikiano huu uliodumu kwa miaka mingi sasa, Benki ya NBC tumekuwa mstari wa mbele katika kubuni huduma mbalimbali za kifedha zinazolenga kurahisha utoaji wa huduma kwenye hifadhi mbalimbali zilizopo hapa nchini.’’
“Zaidi pia tumekuwa tukiwawezesha wadau mbalimbali wa sekta hii kupitia huduma zetu mbalimbali zilizobuniwa mahususi kwa ajili yao ikiwemo mikopo ya fedha, huduma za bima mbalimbali pamoja na huduma za malipo kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia mashine zetu za kufanyia miamala yaani ‘NBC POS Machine‘’ alisema.
Aliongeza kuwa kupitia huduma yake ya kidigitali inayofahamika kama ‘NBC Connect’, benki hiyo imekuwa ikiiwezesha TANAPA na masharika mbalimbali yanayohudumia sekta hiyo kupata huduma za kibenki kwa njia ya mtandao.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Waziri, Balozi Dkt. Chana aliupongeza uongozi wa hifadhi hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za fedha kwa kuendelea kuboresha huduma zake kwa watalii wanaotembelea hifadhi hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri Chana, jitihada za serikali zinazoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na wadau hao, zimechochea ongezeko kubwa la watalii wanaoingia nchini ambapo mwaka wa fedha 2023/24 idadi ya watalii wakimataifa walioingia nchini iliongezeka kwa asilimia 96 kutoka kutoka watalii 900,022 walioingia nchini mwaka 2021 hadi kufikia watalii mil 1.8 mwaka 2023.
‘’Kwa hifadhi hii ya Taifa ya Mikumi, mwaka 2023/24 jumla ya watalii 138,000 wametembelea hifadhi kutoka watalii kutoka watalii 46, 517 mwaka 2020/21, sawa na ongezeko la asilimia 198.48. Ongezeko hili ni jitihaza za pamoja baina ya serikali, hifadhi na wadau wote wakiwemo wananchi wanaozunguka hifadhi hizi…hongereni sana,’’ alisema.
Akiwa kwenye maadhimisho hayo, Waziri Dkt Chana alipata wasaa wa kutembelea miradi mbalimbali ya inayolenga kuboresha huduma zinazotolewa na hifadhi ya Taifa ya Mikumi ikiwemo ujenzi wa vibanda vya kufikia na kupumzikia wageni (picnic sites), maboresho ya uwanja wa ndege wa Kikoboga uliopo kwenye hifadhi hiyo, ujenzi wa milango ya kuingilia watalii, ujenzi wa kituo cha kutoa taarifa kwa wageni (VIC) na mradi wa kuunganisha umeme wa gridi ya taifa kwenye hifadhi hiyo.
“Kukamilika kwa miradi ya maboresha haya kutaongeza idadi ya watalii na kuwezesha ndege kubwa zaidi kutua Hifadhi ya Mikumi kiasi cha kuweza kupokea wageni 140 na kuwahudumia kwa wakati mmoja,’’ alisema.
Zaidi, Waziri Dkt Chana alibainisha kuwa serikali ipo kwenye mpango wa kujenga lango la kupokelea watalii watakaotembelea hifadhi ya Mikumi kwa njia ya reli ya kisasa ya mwendokasi (SGR) kupitia kituo cha Wilaya ya Kilosa, hatua ambayo itachochea wingi wa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo sambamba na kuchochea ajira kwa wananchi wilayani humo vikiwemo vijiji vya Mbamba na Kilangali.
“Kikubwa tu tuhakikishe maboresho haya yanaenda sambamba na ubora katika utoaji wa huduma zetu. Naomba sana huduma zitolewe kwa kuzingatia misingi ya sheria na kanuni zinazosimamia sekta hii ikiwemo suala zima la utoaji wa ajira kwa watoa huduma za utalii uzingatie sifa muhimu ikiwemo elimu,’’ alisema.
Awali akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Nassoro Juma Kuji alisema kufuatia jitihada mbalimbali za serikali hususani Rais Dkt, Samia katika kuboresha na kutangaza sekta ya utali nchini kumekuwa na ongezeko kubwa la watalii nchini hatua iliyoongeza pia kipato kwa shirika hilo ambapo katika kipindi cha mwaka 2022/23 liliweza kuingiza kiasi cha Sh bilioni 337.5.
Naye, Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi, Agustine Masesa aliwashukuru wadau mbalimbali kwa kujitokeza kufanikisha maadhimisho hayo huku akionyesha kutambua jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau hao katika kuchochea ustawi wa sekta hiyo muhimu,
Mwisho.