Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo leo Jumamosi Julai 15, 2023 ametoa agizo kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuipa kibali kampuni ya kuchakata na kudhibiti taka ya Givorah Recycling Limited cha kuchukua taka katika dampo la Pugu Kinyamwezi ambalo linamilikiwa na halmashauri ya jiji hilo.
Waziri Jafo ametoa agizo hilo katika uzinduzi wa kiwanda hiko kilichopo Kata ya Mtoni wilayani Temeke jijini Dar es Salaam mara baada ya kupokea changamoto iliyowasilishwa kwake kwamba kiwanda hiko ufanisi wake unazuiwa na upatikanaji wa malighafi taka ambazo wanapokwenda kuchukua katika sehemu zinapopatikana hususan katika dampo la Pugu Kinyamwezi huombwa kibali ili hali wao wanasaidia katika uhifadhi wa mazingira na udhibiti wa taka.
Waziri Jafo ameendelea kwa kusema kuwa, Jafo ‘Givorah ni miongoni mwa kampuni ambazo zimetekeleza sheria za nchi , na kukikidhi vigezo vya mazingira hatua ambayo inawezesha kupata cheti cha mazingira (Environmental Certificate) kinachotolewa na ofisi yake’
Waziri huyo ameeleza kuwa, Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla wake linazalisha taka kati ya tani 6,000 hadi 7,000 kwa siku hivyo kuwepo kwa kampuni ya Givorah ni msaada lakini badala yake ameshangazwa kuambiwa kampuni hiyo changamoto yake ni malighafi taka.
“Jiji la Dar es Salaam linazalisha taka kati ya tani 6,000 hadi 7,000 kwa siku, na jiji la Dar es Salaam niseme ukweli hatuna dampo la kisasa lakini cha ajabu kiwanda cha kuchakata na kudhibiti taka cha Givorah changamoto yake kubwa ni kupata taka kama malighafi” alisema Waziri Jafo na kuongeza
“Nafahamu lile dampo la Pugu Kinyamwezi lipo katika umiliki wa jiji la Dar es Salaam, nilichosikia ni kwamba kampuni ya kuchakata na kudhibiti taka ya Givorah Recycling inahangaikia kupata vibali vya kuruhusiwa kuchukua taka katika dampo la Pugu Kinyamwezi ni maajabu sana, yaani kuna watu wanataka kutusaidia kuchukua taka lakini kibali cha kuchukua taka hakitoki”
Kufuatia hilo Waziri Jafo ametoa agizo kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hadi kufikia Julai 30, mwaka huu kampuni ya Givorah Recycling iwe imepata kibali .
Vile vile Waziri Jafo ametoa rai kwa kampuni hiyo kuwa na vihifadhi taka (dust bin) katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye taasisi za elimu, hospitalini, sokoni, kwenye mitaa na maeneo mengine ili kuwawezesha kupata malighafi wanayotaka kwa ajili ya uzalishaji.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni ya Givorah Recycling Limited , mwanasheria wa kampuni hiyo Wakili Shehzada Walli ameeleza kuwa, kampuni hiyo imeweza kukusanya asilimia 30 ya taka zilizozalishwa katika kipindi cha maonesho ya biashara (Sabasaba) mwaka huu na kuongeza kuwa kama si wao kukusanya taka hizo zingekweda dampo na hata kuchafua mazingira.
Wakili Walli ameongeza kuwa, changamoto yao kuu wanayopata ambayo pia ni ya kushangaza ni kwamba badala ya jamii kuisaidia kampuni kukusanya taka bure wao wanataka kuuza taka zao jambo linalopelekea kampuni kupata shida sana inapokwenda kukusanya taka na kupunguza ufanisi katika uzalishaji.
Kufuatia hilo Wakili Walli ameiomba serikali kupitia Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira iwasaidie kutoa elimu kwa wananchi kwamba kampuni yao inatoa mchango katika kulinda na kusafisha mazingira na hivyo wawaunge mkono na wawape ushirikiano.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya amesema kwa siku moja taka zinazozalishwa ndani ya manispaa hiyo ni tani 1,400, taka zinazotolewa kwa siku ni tani 964 na huku taka ambazo hazipati udhibiti kabisa kwa siku ni tani 379.
Mabelya ameongeza kuwa, na dampo wanalolitegemea la Pugu Kinyamwezi limezidiwa na hivyo ujio wa kampuni ya Givorah Recycling imekuwa ni mkombozi katika halmashauri yetu ya Temeke na kuahidi kushirikiana na kampuni hiyo.
Akiongea kwa niaba ya wananchi, Abdallah Mtinika ambaye pia ni mstahiki Meya wa manispaa ya Temeke amesema ujio wa kampuni ya Givorah Recycling ni neema na faida kwa wana Temeke ambao ameahidi kuwalinda na kushirikiana nao katika utendaji kazi wao wa kila siku na kwamba watakuwa wanawatembelea mara kwa mara ili kuwasikiliza person changamoto zao na kujua mwenendo wao katika uzalishaji.
Mtinika ameongeza kuwa, miji mingi iliyofanikiwa duniani na kuonekana inapendeza jambo hilo linatokana na mambo mawili makubwa ambayo ni usimamizi thabiti wa usafi na udhibiti wa taka.
Givorah Recycling Limited ni kampuni inayojishughulisha na ukusanyaji na udhibiti wa taka zote ambazo zinazoweza kutumika tena ikiwa na uwezo wa kurejeleza (recycle) taka hadi tani 1,000 kwa siku.
Kampuni hiyo ambayo ilianzishwa nchini India ipo pia katika nchi za Marekani, Ulaya, Falme za Kiarabu na mwaka huu imeanzishwa rasmi nchini Tanzania.