NI Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Seleman Jafo amesema Athari za mabadiliko ya Tabianchi zinaonekana dhahiri katika maeneo mbalimbali nchini na kusema kuwa ipo haja ya kuongeza jitihada za dhati katika kukabiliana nayo.
Waziri Jafo ameyasema hayo hii leo mjini Glasgow Scotland katika Mkutano wa 26 wa Nchi wa Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
mezitaja athari hizo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kulikosababisha kisiwa cha Maziwe Wilaya ya Pangani na kisiwa cha Fungu la Nyani Wilaya ya Rufiji kumezwa na maji ya bahari na kuongezeka kwa kina cha maji kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.
“Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi Ili kukabiliana na athari hizi ambazo zinatishia kurudisha nyuma juhudi za serikali za miongo kadhaa za kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa watu wake” Jafo alisisitiza.
Amesisitiza kuwa katika mkutano unaoendea viongozi wa mataifa makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa mataifa yao ndio chanzo cha uzalishaji wa hewa ya ukaa wameonyesha nia ya dhati ya kutekeleza makubaliano waliojiwekea ya kutoa fedha kwa wakati ili kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Amesema mataifa hayo yanawajibika kutokana na makubaliano ya Mkataba wa Paris ambao unazitaka nchi zilizoendelea kutoa kiasi cha Dola Bilioni Mia moja kila mwaka kwa nchi zinazoendelea ili ziweze kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
“Tunadhamiria na kusisitiza kuwa sasa tutoke kwenye maneno na twende kwenye vitendo, wenye jukumu la kutoa fedha watoe ili miradi mbalimbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi iweze kutekelezeka kwa wakati” Jafo alisisitiza.
DRONE VIDEO: DARAJA LA TANZANITE, JPM ENZI ZA UHAI WAKE ALIYASEMA HAYA