Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini kwa kushirikiana na kampuni ya Oryx gas wamegawa bure mitungi ya gesi 500 pamoja na majiko yake kwa Baba na Mama Lishe wa Jimbo hilo kwa lengo la kuwawezesha kurahisha shughuli zao za kuandaa chakula sambamba na kulinda afya zao.
Akizungumza leo Julai 13,2024 wakati wa kugawa mitungi hiyo, Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoite Araman amesema mitungi hiyo 500 ya gesi ya oryx na majiko yake yamegharimu Sh.milioni 41 na kwamba wataendeela kufuata maelekezo ya serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan inayohamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuendeela kugawa mitungi hiyo kwa wananchi wa makundi mbalimbali.
Amesema Oryx Gas wanaamini kupika kwa gesi kunalinda mazingira kwa kuacha kukata kuni na mkaa lakini inalinda afya kwa kuwaepusha kuvuta moshi na mvuke unaoathiri mapafu na afya yao.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Athony Mavunde amesema wanashukuru kwa kupata majiko hayo huku akieleza na wao wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaenzi kampeni ya kutunza mazingira hasa kwa kuwa na mipango mbalimbali ili wananchi wengi wasitumie nishati ya kuni na mkaa ambayo kwa kiwango kikubwa inaharibu mazingira.
Awali Mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini Alhaj Jabiri Shekimweri amepomngeza Waziri Mavunde kwa jinsi anavyojitoa kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini wakiwemo Baba na Mama Lishe huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza ni vema walipewa mitungi ya gesi na majiko yake kuhakikisha wanaitumia vema gesi hiyo ili wasipate madhara.