Waziri wa Ujenzi Prof. Makame Mbarawa leo June 10,2023 amewasilisha Bungeni maelezo ya awali kuhusu mapendekezo ya kuridhia mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa Bandari Tanzania ambapo amesema manufaa ambayo yanatarajiwa kupatikana iwapo Bunge litaridhia azimio hilo ni pamoja na kuongezeka kwa Mapato ya Serikali yatokanayo na Kodi ya Forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa Bandarini kutoka Tsh. Trilioni 7.76 za mwaka 2021/22 hadi Tsh. Trilioni 26.7 za mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la 244%.
“Manufaa mengine ni kuongezeka kwa shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 158, kuongezeja kwa ajira zinazotokana na shughuli za Bandari kutoka 28,990 mwaka 2021/22 hadi ajira 71,907 ifikapo mwaka 2032/33, sawa na ongezeko la asilimia 148”
“Maboresho ya maeneo ya kuhudumia shehena ya makasha na kuweka mitambo yenye Teknolojia ya kisasa, kuendeleza eneo la kuhifadhia mizigo la Bandari Kavu kwa kuweka miundombinu ya kisasa ya kuhudumia aina zote za shehena, maboresho ya magati ya kuhudumia Majahazi na Abiria ikiwa ni pamoja na kushawishi uingiaji wa meli kubwa za kitalii zitakazo ongeza idadi ya Watalii nchini na kuongeza pato la Taifa”
“Kusimika Mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya shughuli za bandari na kuwaunganisha wadau wake, Mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TPA katika Bandari zote, Uanzishwaji wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi/Viwanda na kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi zikiwemo Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, kuchagiza shughuli za Viwanda na Biashara; kuchagiza ukuaji wa sekta ndogo za usafirishaji kwa njia ya reli (SGR, TAZARA na MGR) na barabara, Watanzania kunufaika na teknolojia na ujuzi wa uendeshaji wa bandari kisasa na kujenga mahusiano ya kidiplomasia”