Waziri wa Ujenzi Prof. Makame Mbarawa leo June 10,2023 amewasilisha Bungeni maelezo ya awali kuhusu mapendekezo ya kuridhia mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa Bandari Tanzania ambapo amesema waliamua kuchagua kufanya majadiliano na Kampuni ya DP World kwakuaa ina uzoefu wa kuendesha Bandari sita Afrika na Bandari zaidi ya 30 Duniani kote kwa ufanisi mkubwa.
“Ili kutatua changamoto za Bandari zilizopo na kwa kuzingatia dhima ya Serikali ya kuboresha Sekta ya Bandari nchini ili kuongeza ufanisi na mchango wa Sekta ya Bandari katika mapato ya nchi, ajira na kuchagiza sekta nyingine za kiuchumi, Serikali ilifanya maamuzi ya kutafuta Wawekezaji wapya wanao endana na dhima ya Serikali”
“Hatua hizo zilihusisha kupokea mapendekezo ya Wawekezaji mbalimbali wakiwemo kampuni ya Hutchson (Hong Kong), Antewerp/Brugge (Belgium), PSA International (Singapore), DP World (Dubai), Abu Dhabi Ports (Abu Dhabi), Adani Ports and Logistics (Mundra-India), Kampuni ya CMA-CGM (France) pamoja na Kampuni ya Maersk (Denmark)”
“Serikali iliamua kuanzisha majadiliano na kampuni ya DP World kwa kuzingatia uzoefu wake katika uendeshaji wa shughuli za Bandari Barani Afrika, Asia, Ulaya na Amerika ya Kaskazini na Kusini, kwa upande wa makampuni mengine ambayo TPA ilipokea mapendekezo yao, yalionesha nia ya kuwekeza bandarini pekee na sio kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji”
“Pia, baadhi ya makampuni hayo hayana uzoefu wa kuendesha shughuli za Bandari Afrika wakati Kampuni ya DP World inaendesha takriban Bandari 6 Afrika na Bandari zaidi ya 30 Duniani kote kwa ufanisi mkubwa, kwa kuzingatia nia ya Serikali kuvutia uwekezaji nchini, wakati wa maonesho ya Dubai Expo 2020 tarehe 28 Februari, 2022 Hati za Makubaliano takriban 30 zilisainiwa baina ya Taasisi za Serikali ya Tanzania na Sekta binafsi na Taasisi za Serikali za Dubai kwa lengo la kuvutia uwekezaji nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Nchi”