Waziri wa Ujenzi Prof. Makame Mbarawa leo June 10,2023 amewasilisha Bungeni maelezo ya awali kuhusu mapendekezo ya kuridhia mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa Bandari Tanzania ambapo amesema kutokana na ufanisi mdogo wa Bandari ya Dar es salaam kwa sasa gharama za meli kusubiri nangani kwa siku moja ni takriban Dola za Marekani 25,000, sawa na takriban Shilingi milioni 58 kwa siku.
“Athari za kutokuwa na ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam ni pamoja na meli kusubiri muda mrefu nangani ambako kunasababisha kuongezeka kwa gharama ya kutumia bandari ya Dar es Salaam, kwa mfano gharama za meli kusubiri nangani kwa siku moja ni takriban Dola za Marekani 25,000, sawa na takriban Shilingi milioni 58 kwa siku, meli kutumia muda mrefu kupakia na kupakua shehena gatini kwa wastani wa siku 5 ikilinganishwa na siku 1 inayokubalika kimataifa, meli kubwa kutokuja katika bandari ya Dar es Salaam kutokana na kuchukua muda mrefu kuhudumiwa”
“Hali hii husababisha bandari yetu kuwa Bandari inayolishwa shehena na Bandari zingine na kuongeza gharama ya kutumia Bandari hiyo na kuikosesha nchi mapato ambayo yangeweza kutumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini ambayo ingesaidia kukuza uchumi na kuboresha huduma za Wananchi”
“Pia, kunaongeza gharama katika mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka nje ya nchi, kupitia katika Bandari yetu kwenda nchi za jirani zinazotumia Bandari hiyo, kwa mfano, gharama ya kusafirisha kasha moja kutoka nje ya nchi kwenda DRC zinafikia takriban Dola za Marekani kati ya 8,500 hadi 12,000, hii ni gharama kubwa sana ikilinganishwa na Bandari shindani”