Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Septemba 29, 2024 alifanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Amref Health Africa Dkt. Githinji Gitahi, kando ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 79) ambao alishiriki kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Jijini New York,
Katika mazungumzo hayo Mheshimiwa Majaliwa alilipongeza shirika hilo kwa kazi kubwa inayofanya kwenye sekta ya afya nchini Tanzania na alimuahidi Mkurugenzi Mtendaji huyo kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano ili mipango na malengo ya shirika hilo ya kuisaidia sekta ya nchini yaendelee kufanikiwa.
Amesema kuwa jitihada ambazo shirika hilo limekuwa likizifanya kwenya sekta ya afya nchini Tanzania zimeendelea kuzaa matunda na kuwezesha kuwafikia watanzania wengi kwenye huduma ya afya
“Kwenye hili niendelee kukuomba uamini kwamba Tanzania ni rafiki wa kweli kwenye mipango ya Shirika, mafanikio ya kupunguza vifo vya mama na mtoto yanatokana na mahusiano yetu, tunataka tupunguze zaidi na ikiwezekana tuiondoe, inaweza kuwa sio rahisi lakini ishuke chini ya robo”
Kwa upande wake, Dkt. Githinji ameipongeza Serikali ya Tanzania Serikali kwa kupunguza Vifo vya Mama hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 ikiwa ni punguzo la asilimia 80 kutoka 2016.
“Hii ni chini ya wastani wa kimataifa wa vifo 211 kwa kila vizazi hai 100,000 na wastani wa kikanda wa vifo 391 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa Kusini na Mashariki mwa Afrika”. Alisema Gitahi
Amref imekuwa ikishirikiana na Tanzania kwenye maeneo ya ujenzi wa mifumo ya afya, Kujengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii, magonjwa ya mlipuko, magonjwa ya kifua kikuu, ukimwi na malaria na eneo la afya ya mama na mtoto”
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu.