Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Nishati iratibu ununuzi wa mafuta kutoka Mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa ili yachukuliwe kutokea Tanga badala ya Dar es Salaam.
Ametoa agizo hilo leo Jumamosi, Julai Mosi, 2023 mara baada ya kukagua uboreshaji wa bandari ya Tanga na hifadhi ya mafuta kwenye matenki ya GBP, eneo la Raskazoni, Jijini Tanga.
“Mikoa ya Mara, Mwanza, Manyara, Arusha, Kilimanjaro inafuata mafuta Dar es Salaam sababu ya mazoea lakini upatikanaji rahisi ni hapa Tanga, upatikanaji wa haraka sababu ya teknolojia ni hapa Tanga, Wizara ya Nishati watekeleze maelekezo haya ili wauzaji wa mafuta wayafuate Tanga”.
Waziri Mkuu amesema endapo makampuni yote ya Mikoa ya Kaskazini yatachukulia mafuta Tanga, uchumi wa Mkoa huo utakua kwa haraka.
Waziri Mkuu amesema uwekezaji uliofanyika ni mkubwa kwani matenki yaliyopo yanaweza kupokea mafuta moja kwa moja kutoka bandarini na kuhifadhi lita hadi milioni 200….“Huu ni mkakati wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuendeleza uchumi wa nchi yetu. Wakati Serikali inaongeza uwezo wa kusimamisha meli zaidi bandarini, tutahakikisha kuwa uwekezaji huu unaleta faida kwa mwekezaji na unaongeza ajira kwa Wana Tanga”