Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amezindua mashine ya kuchanganya virutubisho kwenye vyakula na kuwaomba wadau wote wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizo ili kuwezesha mashine hizo kuzalishwa kwa wingi kutumika katika maeneo yote hapa nchini.
Mashine iliyozinduliwa inatumika kuongeza virutubisho muhimu katika vyakula hususan unga wa mahindi, virutubisho hivyo ni pamoja na vitamin B na folic acid ambayo zinasaidia kwenye ukuaji wa watoto na kuzia kuzaliwa na changamoto za ulemavu ikiwemo mgongo wazi na vichwa vikubwa.
Waziri Mkuu amezindua mashine hiyo leo (Alhamisi, Oktoba 26, 2023) wakati akitembelea mabanda ya maonesho kabla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Tisa wa Wadau wa Lishe nchini uliofanyika katika Jijini Arusha. “Ninawapongeza sana wote waliowezesha kufikia hatua hii sambamba na mchango wa Shirika la GAIN, SIDO na DIT kwa kuwezesha kazi hii kukamilika.”
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wadau hao wahakikishe virutubisho vinavyotumika katika mashine hizo vinazalishwa nchini ili kuondokana na utegemezi wa kuviagiza kutoka nje ya nchi.
Aidha, Waziri Mkuu amewahakikishia wadau hao kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan siku zote itaendelea kuunga mkono juhudi hizi ili kuhakikisha zinakuwa endelevu. Kadhalika,
Waziri Mkuu amesisitza Ofisi ya Rais – TAMISEMI ihakikishe kuwa mikataba ya lishe kati ya Mheshimiwa Rais na Wakuu wa Mikoa inatekelezwa kikamilifu na kuwa na tija. “Fanyeni ufuatiliaji wa karibu na kutoa taarifa za utekelezaji mara kwa mara.”
“Watendaji Wakuu wote wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Umma na Binafsi pamoja na Wadau wa Maendeleo na Asasi za Kijamii wekeni malengo ya lishe katika mipango yenu pamoja na kutenga fedha za utekelezaji kila mwaka kwa mujibu wa viwango tulivyojiwekea.”