Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa Mnara wa Mashujaa uliopo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ikiwa ni maandalizi ya Siku ya Mashujaa itakayofanyika Dodoma, Julai 25, 2024.
Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi wa mnara huo Majaliwa amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi na amemtaka mkandarasi wa mnara huo ambaye ni Suma JKT kukamilisha ujenzi kwa viwango na ubora ifikapo Julai 22 mwaka huu.
Naye, mshauri elekezi kiongozi, Dkt. Ladislaus Mrema amesema kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa eneo hilo la mnara unajumuisha ujenzi wa uwanja wa gwaride, ngazi, njia za watu wenye mahitaji maalum pamoja na kitako cha mnara na bushati eneo la kuzunguka mnara “Mpaka sasa mradi huu umefikia asilimia 84”
Siku ya Mashujaa itafanyika Julai 25, mwaka huu na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.