WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wamiliki wa malori nchini wawajali madereva na wahudumu wa magari hayo ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi yao.
Amesema uanzishwaji wa kanzidata ya taarifa za madereva utawawezesha wamiliki hao kutumia taarifa hizo kwa lengo la kusimamia usalama wa madereva pamoja na kufuatilia mienendo na ufanisi wao.
“Katika hili, niwasisitize kuhusu kuzingatia usalama na maslahi ya madereva wenu ambao kimsingi ni walinzi wa mitaji yenu kupitia vyombo ambavyo mmewapa dhamana ya kuviendesha. Haki iende na wajibu, yaani mnataka wawatumikie, kwa hiyo na ninyi mboreshe maslahi yao,” amesisitiza.
Ametoa wito huo wakati akizungumza na wadau wa sekta ya usafirishaji waliohudhuria uzinduzi wa kanzidata ya madereva wa malori nchini leo (Alhamisi, Desemba 14, 2023) jijini Dar es Salaam. Kanzidata hiyo imeandaliwa na Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA).
Akizungumza na wadau wa sekta hiyo, Waziri Mkuu amesema azma ya Serikali ya awamu ya sita ni kuendeleza sekta hiyo ili iweze kuharakisha ukuaji wa uchumi. “Hatua iliyofikiwa leo ni kuhakikisha makao makuu ya mikoa yote inafikika kwa lami na shoroba zote za Kusini, Kati na Kaskazini kuelekea nchi za jirani za Kenya, Kongo, Malawi na Zambia zinapitika bila shida.”
Akielezea maboresho ya sekta hiyo, Waziri Mkuu amesema Serikali tayari imekamilisha ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa km. 2,183.82 na km. 14,348 za changarawe. Licha ya hayo imekuwa ikiendelea na matengenezo ya kawaida ili kuzifanya barabara zetu ziweze kupitika wakati wote.
Sambamba na maboresho hayo ya barabara, Waziri Mku amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) unaoambatana na uundaji wa vichwa 17 vya treni, uboreshaji wa bandari za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na kwenye maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa ambapo muda wa kugomboa mizigo bandarini umepungua kutoka siku 14 hadi siku sita.
“Uimarishwaji wa sekta hizi haulengi kuua usafirishaji wa malori kwani ujenzi upanuzi wa bandari zetu, utaleta mizigo mingi zaidi na kazi ya usafirishaji itafanywa na ninyi,” amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu alipokea hundi kutoka kwa wanachama wa TATOA wenye thamani ya sh. milioni 100 ikiwa ni mchango wao kwa waathirika wa maafa ya mafuriko huko Katesh, wilayani Hanang, mkoani Manyara.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, aliwapongeza viongozi wa TATOA kwa ubunifu wao mkubwa wa kuamua kuandaa kanzidata hiyo.
Alisema Serikali inao mfumo wa kusajili madereva ulioko chini ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ambao umeshasajili madereva 19,709 wakiwemo wa mabasi na malori. “Kanzidata hii itatumiwa pia na Serikali kufuatiulia mwenendo wa madereva wa malori,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa TATOA, Elias Lukumay alisema kuundwa kwa kanzidata hiyo kutasaidia mambo mengi kwani kitakuwa ni chombo chenye nguvu kwa vile kitakuwa na taarifa zaidi ya majina na leseni zao.
“Chombo hiki kitatoa taarifa baina ya madereva na wamiliki wa malori, pia kitaondoa changamoto wa watu wasio waaminifu na kitakuwa alama ya usalama kati ya dereva, mmiliki wa lori na mteja,” alisema.
Awali, Mwakilishi wa Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Bw. Louis Manzombi Kisombo alisema suala la mawasiliano ni pana sana na akaomba suala la kuunda Kamati ya Pamoja ya kufuatilia malalamiko ya madereva lifanyiwe kazi mapema ifikapo Januari, 2024.
Alisema Kamati hiyo itakayokuwa na jukumu la kupokea malalamiko ya pande zote, itapaswa kuwa inakutana walau kila baada ya miezi mitatu na kwamba ubalozi wao uko tayari kutoa ushirikiano kwa Kamati hiyo.