Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema kwa sasa Serikali imeruhusu Wafanyabiashara wa sukari na wenye viwanda kuingiza sukari kutoka nje ya Nchi ili kupunguza makali ya upatikanaji wa sukari kutokana na viwanda vingi Nchini kusimamisha uzalishaji baada ya mashamba kujaa maji.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Bungeni Jijini Dodoma leo wakati akijibu swali la Mhandisi Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Nyasa, aliyetaka kujua hali ya upatikanaji wa sukari Nchini hasa kuelekea kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Majaliwa amesema “Ni kweli tuna upungufu wa sukari na upungufu huu unatokana na kuwepo kwa mvua nyingi ambazo maeneo yetu ya mashamba ya miwa inayozalisha sukari maji yamejaa kiasi cha kwamba wale Wamiliki wa mashamba hawawezi kutoa miwa kutoka mashambani kwenda viwandani na kweli viwanda vimebaki havina sukari”
“Wizara imetoa vibali kwa Wafanyabiashara wa sukari ikiwemo Wazalishaji wenyewe kuingiza sukari nchini zaidi ya tani laki moja na taarifa nilizonazo kutoka Wizara ya Kilimo tayari tumeanza kupata sukari kutoka nje na hii itaendelea kupunguza makali ya kukosekana kwa sukari Nchini”