Waziri Mkuu wa India Narendra Modi Jumapili alitoa wito kwa Umoja wa Afrika (AU) kuwa mwanachama wa G20, klabu ya nchi tajiri zaidi duniani zinazotarajiwa kukutana nchini India mwezi Septemba.
“Tumealika Umoja wa Afrika kwa wazo la kuupa hadhi ya mwanachama wa kudumu” wa G20, Narendra Modi alisema wakati wa kongamano la biashara la B20 ambalo lilifanyika kabla ya mkutano wa kilele wa G20 mnamo Septemba 9 na 10.
Mwezi Disemba, Rais wa Marekani Joe Biden alikuwa tayari ameeleza matakwa ya Umoja wa Afrika kujiunga na G20 kama mwanachama wa kudumu, akihakikishia kwamba “itatokea”.
Ni nchi moja tu ya Kiafrika, Afrika Kusini, ambayo kwa sasa ni mwanachama wa G20, ambayo inaleta pamoja nchi 19 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani pamoja na Umoja wa Ulaya, unaowakilisha 85% ya Pato la Taifa la dunia na theluthi mbili ya watu wote duniani.
Ikiwa na makao yake mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, AU ina nchi wanachama 55, jumla ya dola trilioni tatu katika Pato la Taifa.
Waziri Mkuu wa India pia alithibitisha kuwa nchi yake, mpinzani mkubwa wa Uchina, ilikuwa na uwezo wa kufidia shida za usambazaji zinazosababishwa na mzozo wa Covid.
India ndio “suluhisho” la kuunda “mnyororo wa kuaminika wa usambazaji wa kimataifa”, kwa sababu “ulimwengu umebadilika sana baada ya Covid-19,” Bw Modi alisema.
Alhamisi katika mkutano wa kilele wa BRICS (kundi la nchi kubwa zinazoinukia) nchini Afrika Kusini, Bw. Modi alizungumza ana kwa ana na Rais wa China Xi Jinping.