Waziri wa Fedha na Mipango Dokta Philip Mpango amepokea gawio la Bilioni 17 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Mpango aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali na kwa kupata faida katika biashara yake katika kipindi cha mwaka 2019/20 ambayo yamepelekea kuongezeka kwa gawio kwa Wanahisa ikiwamo Serikali.
“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki yetu ya CRDB inazidi kuimarika zaidi kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii” Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2020/2021 hususan sekta ya afya.
“Kipekee kabisa niipongeze Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB kwa kazi nzuri mnayoifanya,” Dkt. Mpango.
Aidha, aliipongeza Benki ya CRDB kwa matokeo mazuri ya biashara iliyopata katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2020 ambapo faida ya Benki imeongezeka kwa asilimia 15 kufikia shilingi bilioni 70.4 kutoka TZS bilioni 61.1 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2019,
Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa taasisi za fedha katika maendeleo ya taifa, Dkt. Mpango aliipongeza Benki ya CRDB kwa kupunguza riba katika mikopo kutoka asilimia 24 kufikia wastani wa asilimia 18 na 14 ili kuchochea shughuli za maendeleo nchini.
“Niwapongeze kwa kupunguza riba katika mikopo, hiki kimekuwa kilio cha muda mrefu cha Serikali kwa mabenki nchini, niyasihi mabenki mengine kufuata nyayo hizi za Benki ya CRDB,” Dkt. Mpango.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, alisema kuwa gawio hilo ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 120.1 baada ya kodi ambayo Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu imeipata katika mwaka wa fedha 2019/2020 na kuahidi kuwa Benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji ya wanahisa wake na wananchi kwa ujumla.
“Katika Mkutano wa Wanahisa uliofanyika kidijitali mwezi Juni mwaka huu, Wanahisa wa Benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la shilingi 17 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 112.5 na hivyo kufanya gawio la mwaka huu kufikia jumla ya shilingi bilioni 44.4,” Dkt. Laay.
Aidha, Dkt. Laay aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji mzuri ambao umeiwezesha Benki ya CRDB kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo ili kukuza uchumi wa nchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alimhakikishia Dokta Mpango kuwa Benki ya CRDB kupitia kauli mbiu yake ya “Tupo Tayari” itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha nchini huku akielezea kuwa benki hiyo sasa hivi imejikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidijitali ya kutolea huduma.
Akipokea gawio kutokana na uwekezaji wa Halmashauri za Mbinga, Lindi, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe, Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jaffo alizihimiza halmashauri nyingine nchini kuwekeza katika hisa ili kupanua wigo wa mapato katika halmashauri zao.
Serikali ndio mwanahisa mkubwa ndani ya Benki ya CRDB kutokana na kuwa na umiliki wa asilimia 21 kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA kushirikiana na Serikali ya Denmark, huku taasisi na mashirika ya umma yakiwa na umiliki wa hisa za asilimia 17.1.
HAHAA! USIYOYAJUA KUMHUSU BUSHMAN, UTAJIRI WAKE, KUFILISIKA, HAJUI PESA WALA HESABAU,