Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewahimiza wawekezaji kutoka kila pembe ya dunia, kuwekeza katika sekta ya nishati ya umeme nchini Tanzania, ili kuzalisha nishati ya kutosha na ya uhakika ambayo itauzwa katika nchi mbalimbali ikiwa ni njia ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa nishati hiyo katika Bara la Afrika.
Dkt. Nchemba ametoa wito huo Jijini Washington D.C, nchini Marekani, wakati akizungumza kwenye mkutano wa Mawaziri wa Fedha kutoka nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika, waliojadili kuhusu usalama wa nishati na namna ya kuishirikisha sekta binafsi kuwekeza kwenye uzalishaji wa nishati ya umeme na kutumia pia changamoto hiyo kama fursa ya kufanya biashara ya kuuziana nishati hiyo,
Alisema kuwa nishati ya umeme ni muhimu katika kusisimua na kukuza uchumi wa nchi kwakuwa ni chanzo cha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali na kwamba kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo kutachochea ukuaji wa uchumi, maisha ya watu na kuziwezesha nchi kutekeleza lengo namba 7 la malengo endelevu ya milenia linalohimiza upatikanaji wa nishati kwa bei nafuu, ya uhakika na ya kisasa ifikapo mwaka 2030.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania imeweka sera na mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo kubadilisha baadhi ya sheria na taratibu zilizokuwa zikikwaza uwekezaji na kwamba hatua hiyo inatoa fursa ya kuvutia uwekezaji katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Alisema kuwa hivi sasa Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya kuzalisha umeme ukiwemo mradi wa Bwawa la Nyerere ambalo litazalisha megawati 2,115, pamoja na kujenga njia ya umeme ya 400kV yenye urefu wa kilometa 1,300 itakayounganisha nchi za mashariki na kusini mwa Afrika, ambapo tayari kilometa 900 za njia hiyo zimejengwa na umekamilika.
“Serikali itaishirikisha kikamilifu sekta binafsi kuzalisha umeme wa kutosha na wa uhakika ili tuweze kufikia lengo tulilojiwekea la kuzalisha megawati 10,000 za umeme ifikapo mwaka 2025 na tutaendelea kuboresha sheria zetu kuhusu uwekezaji ambazo tunaamini zitavutia zaidi uwekezaji nchini, na nitumie fursa hii kuwakaribisha wawekezaji wote mje kuwekeza ili kuziba pengo la uzalishaji wa umeme lililopo” alisema Dkt. Nchemba.