Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema wizara kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Februari, 2024 imepata mafanikio katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia sekta za utamaduni, sanaa na michezo.
Hayo yamesemwa katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bw. Gerson Msigwa kwenye ufunguzi wa Baraza la pili la Wafanyakazi lililofanyika Februari 27, 2024 Jijini Dodoma.
Akitaja mafanikio hayo, Katibu Mkuu Msigwa amesema katika kipindi hicho wizara imefanikiwa kuendelea Kubidhaisha lugha ya Kiswahili duniani kwa kuongeza vituo, kuendelea kuhifadhi Historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika kupitia Kituo cha Urithi na Ukombozi wa Bara la Afrika pamoja na kufanikiwa kusimikwa kwa Sanamu la Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika nchini Ethiopia.
” Katika kipindi hichi nchi yetu ilipata nafasi ya kupewa uwenyeji wa Mashindano ya AFCON mwaka 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, kuanza ujenzi wa kituo cha umahiri wa michezo katika Chuo cha Michezo Malya, ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa pamoja ujenzi wa vituo vya kupumzikia Dar es Salaam na Dodoma.
Katibu Mkuu Msigwa amewapongeza watumishi wa wizara hiyo kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo ambayo yameleta mafanikio yanayoonekana hivi sasa.
Aidha, Katibu Mkuu Msigwa amewahimiza watumishi wa wizara hiyo kuendelea kuhakikisha kila mtanzania mwenye kipaji cha sanaa na michezo anapata nafasi ya kuonesha kipaji hicho, kushirikiana katika kazi, kupendana, kusaidiana, kulindana na kuweka mazingira wezeshi katika kukuza sekta za utamaduni, sanaa na michezo.