Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amehimiza ushirikiano baina ya ofisi hiyo na Wizara ya Kilimo ili kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.
Prof. Ndalichako akizungumza kwenye hafla ya mapokezi ya vijana 268 wanufaika wa programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT), katika Shamba la pamoja la Chinangali II Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, amesema na serikali imeanzisha programu hiyo ili kupunguza tatizo la ajira, hivyo wakiwezeshwa kufanya kilimo biashara wataweza kujiajiri, kuajiri wenzao na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika pato la Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema vijana hao wa BBT wamekabidhiwa vifaa wezeshi vya kilimo pamoja na mashamba na wataanza na kilimo cha alizeti katika eneo hilo la Chinangali II.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, ameeleza kuwa programu hiyo ya Jenga Kesho Iliyo Bora itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kiwango cha upatikanaji wa chakula nchini.