Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa ameipa siku sita kamati maalumu ya kutatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa kijiji cha Sikaungu wilaya Sumbawanga mkoani Rukwa na shamba linalomilikiwa na Shirika la Efatha.
Waziri silaa ametoa maelekezo hayo wakati alipofanya ziara katika kijiji hicho ili kutatua mgogoro wa ardhi wa muda mrefu ambao umekuwa ukisababisha maafa kila mara.
Kamati hiyo ya utatuzi wa mgogoro huo ambayo imeundwa na Waziri Silaa inajumuisha wataalamu kutoka Makao Makuu Dodoma ikiongozwa na Kamishna wa Ardhi Mathew Nhonge, Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Rukwa, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, TAKUKURU pamoja na wawakilishi wa wananchi.
Waziri Silaa amesema hadi kufikia ijumaa ijayo ya tarehe 24 Novemba 2023 kamati hiyo iwe imekamilisha taarifa hiyo ambapo yeye mwenyewe atakuja kutoa maamuzi ya kile kilichoafikiwa na kamati hiyo ya uchunguzi.
Waziri Silaa ameitaka kamati hiyo kufanya uchambuzi wa kina na kuchunguza historia ya umiliki wa shamba hilo, chanzo cha mgogoro, mipaka ya eneo hilo na umiliki halisi wa shamba hilo pamoja na kutoa mapendekezo.