Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza juhudi za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuondoa changamoto za Muungano.
Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar katika mazungumzo kati yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira Ummy Mwalimu aliyefika Ikulu kwa ajili ya Kujitambulisha.
Rais Dk. Hussein Mwinyi alipongeza hatua hiyo ambayo imekuwa ikifanyiwa kazi kwa makusudi katika kutatua changamoto hizo na kueleza matumaini yake kwamba hatua hiyo italeta mafanikio makubwa kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kuwa mategemeo yake ni kutafutiwa ufumbuzi wa changamoto hizo na kueleza kwamba kwa yake yanayohusu ngazi za juu kwa upande wao wako tayari kuyafanyia kazi ili kufikia pale palipokusudiwa.