Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu leo anazindua Chama cha wataalamu wa TEHAMA katika sekta ya afya(TAHIA) chenye lengo la kukuza nafasi za wataalamu hao kuchangia katika utekelezaji wa Mikakati ya Taifa ya Afya Kidigitali.
Hafla hiyo ilitanguliwa na kongamano la siku mbili la matumizi ya TEHAMA katika sekta ya afya na maonyesho ambayo yalitoa mwanya wa kubadilishana maarifa kuhusu mifumo ya taarifa katika sekta ya afya.
Washirika na serikali walijadili namna ya kuboresha ushirikiano katika mfumo wa taarifa katika sekta ya afya.
Rais wa TAHIA ambaye pia ni Afisa Mkuu wa TEHAMA katika Wizara ya Afya anasema chama hicho kimejipanga kupanua uwezo katika matumizi ya TEHAMA na kuimarisha mifumo ya afya ya Tanzania.
“Sehemu ya malengo makuu ya TAHIA ni kupitia maendeleo ya utekelezaji wa mkakati wa afya wa kidijitali wa Tanzania 2019-2024 na mipango ya uwekezaji kwenye afya ya kidijitali na mabadiliko ya kidijitali katika utoaji wa Huduma ya Afya ya Msingi,’’ anasema, akifafanua dira ya chama.