Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), leo amekutana na Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe, kikiwa ni kikao chake cha kwanza kufanya na uongozi wa Chuo hicho tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.
Katika mazungumzo yake yaliyofanyika Kampasi Kuu- Morogoro, Waziri Mkenda, amehimiza vyuo vikuu vya umma kuwekeza katika utafiti pamoja na kupanua wigo wa mahusiano na Taasisi za kimataifa ili kuwaongezea ujuzi wahadhiri pamoja na kupata uwanda mpana wa taaluma kutoka katika vyuo vingine duniani.
Moja ya mambo ambayo nimejizatiti kuyasimamia kama Waziri wa Elimu, ni Ubora wa Elimu inayotolewa na vyuo vikuu nchini, pamoja na kuendelea kupitia Sera, Miongozo na Kanuni zitakazo tuwezesha kuendelea kuboresha Sekta ya Elimu nchini, ikiwemo mitaala na programu zenye tija alisitiza
Aidha, amehimiza wanataaluma kufungua milango ya kubadilishana ujuzi na taasisi zingine za ndani na nje ya nchi, pamoja na wanataaluma kuwekeza katika uandishi wa miradi ya utafiti na kuichapisha katika majarida yenye ubora na yanayotambulika duniani.
Amewataka viongozi katika Taasisi za Elimu ya Juu, kuwekeza katika elimu kwa kuwasomesha wanataaluma kwenye vyuo vyenye ubora duniani kama ilivyotamkwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo imelenga kuinua ubora wa elimu ya juu nchini.
Pia amewataka kuwatambua wanataaluma wanaofanya vizuri katika uandishi wa machapisho na miradi ya Utafiti, ili kuongeza idadi ya utafiti na machapisho hususani katika fani ya Sayansi na Afya.
Akimkaribisha Waziri wa Elimu, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Lughano Kusiluka, amesema, mpaka sasa Chuo Kikuu Mzumbe kinatoa mafunzo katika maeneo mbalimbali ya ubobevu ikiwemo Sayansi, Teknolojia, Uchumi, Biashara, Mifumo ya Afya, Ununuzi na Ugavi, Sheria, Menejimenti na Utawala na kwamba hadi sasa chuo hicho kina Kampasi tatu Morogoro, Mbeya na Dar es Salaam na wanafunzi zaidi ya elfu kumi na tatu (13,000) kwa ngazi ya Stashahada, Astashahada, Shahada za Awali na Shahada za Umahiri.
Chuo kinaendelea na uwekezaji katika miundombinu kupitia miradi mbalimbali ikiwemo malazi ya wanafunzi na madarasa ili kuongeza wigo wa wanafunzi wanaodahiliwa na chuo hicho kila mwaka.
Katika mkutano huo, Mhe Waziri Mkenda alipata fursa ya kutembelea moja wapo ya mradi unaotekelezwa wa ujenzi wa Hosteli za wanafunzi zilizojengwa kwa ufadhili wa Serikali na kukamilika, na wakati wowote zitaanza kutumika baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kantini. Jumla ya wanafunzi 1024 watanufaika na mradi huo.