Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema katika kuimarisha uthibiti ubora wa Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi Serikali pamoja na mambo mengine itanunua magari matatu kwa ajili ya shughuli za uthibiti ubora wa Shule katika Halmashauri ya Mlele, Tunduma na Serengeti.
Akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2024/2024, Prof. Mkenda amesema “Serikali itafanya tathmini ya jumla katika asasi 6,620 (Shule za awali na Msingi 4,965, Sekondari 1,525, Vyuo vya Ualimu 66, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 14, na Vituo 50 vya elimu ya Watu wazima na mafunzo nje ya mfumo rasmi)”
“Serikali pia itafanya ufuatiliaji na tathmini kwa lengo la kubaini ubora katika uandikishaji, ufundishaji na ujifunzaji, usimamizi na ongozi na kutoa ushauri kwa Walimu wa masomo katika Taasisi 1,010 na itaendelea na ujenzi wa ofisi ya uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlele na ukarabati wa ofisi nne za uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Mpwapwa, Chato, Mpanda na Halmashauri ya Mji – Ifakara na itanunua samani na vitendea kazi katika ofisi 210 (Halmashauri 184 na Mikoa 26) za uthibiti ubora wa Shule”